Home Habari Kuu Rais Ruto kuanza ziara ya siku nne eneo la Nyanza

Rais Ruto kuanza ziara ya siku nne eneo la Nyanza

0
Waziri wa habari, mawasiliano na uchumi wa kidijitali, Eliud Owalo

Rais William Ruto anatarajiwa kuanza ziara ya siku nne ya kimaendeleo katika eneo la Nyanza, kuanzia Ijumaa wiki hii.

Huku akiwahimiza wakazi wa eneo hilo kumkaribisha kiongozi wa taifa katika eneo hilo, waziri wa habari, mawasiliano na uchumi wa kidijitali Eliud Owalo, ametaja ziara hiyo kuwa ya kihistoria katika eneo hilo, alilotaja limesalia nyuma kimaendeleo kwa miaka mingi.

Rais anatarajiwa kuzuru kaunti za Kisumu, Homa Bay, Migori, na Siaya, ambapo atazindua miradi ya maendeleo katika maeneo hayo.

Kulingana na waziri huyo, siku ya Ijumaa Rais atazindua mradi wa samaki wa shilingi bilioni tatu wa  Kabonyo Kanyagwal katika kaunti ya Kisumu.

Mradi huo unajumuisha chuo cha kutoa mafunzo kuhusu samaki, kituo cha utafiti na uvumbuzi na kituo cha ukuzaji samaki. Kulingana  na Owallo, hatua hiyo inalenga kufufua uchumi wa baharini katika eneo la ziwa Victoria.

Rais pia atazindua miradi ya barabara ya Koru-College road, Lake Basin Mall, MV Uhuru II, na miradi ya maji kaunti ya Kisumu.

Katika kaunti ya Homa Bay, Owalo alisema Rais atazindua ujenzi  wa barabara wa Mfangano , Sindo-Magunga, Homa Bay pier na mradi wa maji wa Oyugis.

Owalo alisema Rais atakamilisha ziara yake kwa kuandaa mkutano wa baraza la mawaziri katika ikulu ndogo ya kisumu siku ya Jumatatu.

Aliwasihi wakazi wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi kumkaribisha kiongozi wa taifa, akisema kuwa tangu taifa hili kupata uhuru, hakuna miradi ya maendeleo ya aina hiyo imewahi kuzinduliwa katika eneo hilo.

Website | + posts