Home Habari Kuu Rais Ruto: Kenya ina mazingira bora kwa uwekezaji wa kimataifa

Rais Ruto: Kenya ina mazingira bora kwa uwekezaji wa kimataifa

Alitaja kuanzishwa kwa mfumo mpya wa utozaji ushuru kuwa moja ya hatua ambazo serikali inanuia kutumia kuvutia uwekezaji wa kigeni.  

0
Rais William Ruto akiwa San Francisco nchini Marekani.

Rais William Ruto amesema Kenya imejitolea kuvutia uwekezaji wa kigeni wa hali ya juu humu nchini.

Kiongozi wa taifa alidokeza kuwa serikali inafanya marekebisho yatakayoibadili Kenya kuwa kitovu cha kibiashara katika kanda.

Alitaja kuanzishwa kwa mfumo mpya wa utozaji ushuru kuwa moja ya hatua ambazo serikali inanuia kutumia kuvutia uwekezaji wa kigeni.

“Mazingira bora ya uwekezaji, yatasababisha biashara kuwa na uvumbuzi, kustawi na kubuni fursa zaidi za kiuchumi kwa wananchi,”alisema Rais Ruto.

Rais Ruto akutana na wawekezaji San Francisco nchini Marekani.

Rais aliyasema hayo siku ya Ijumaa wakati wa mkutano wa uwekezaji Silicon Valley, San Francisco, nchini Marekani.

Ruto alisema Kenya imeimarisha masharti yake ya kulinda takwimu sambamba na sheria za kimataifa hasa kuhusu usalama,kawi isiyochafua mazingira na miundo msingi bora.

Kiongozi wa taifa alidokeza kuwa Kenya inawapiga jeki wafanyabiashara kupitia kuanzishwa kwa vituo vya kidijitali katika kila wakilishi wadi hapa nchini.

Balozi wa Marekani humu nchini Meg Whitman, British Robinson, mshirikishi wa uwekezaji barani Afrika, wawekezaji kadhaa na wakuu wa viwanda walihudhuria kikao hicho.

Website | + posts