Home Kimataifa Ruto: Jumuiya ya kimataifa inapaswa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

Ruto: Jumuiya ya kimataifa inapaswa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi

Katika hotuba yake Rais alitoa wito wa kujitolea kimataifa kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabianchi.

0

Rais William Ruto siku ya Ijumaa  alihutubia mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi, COP28 ulioandaliwa jijini Dubai katika Ufalme wa Milki za Kiarabu, UAE.

Katika hotuba yake, Ruto alitoa wito wa kujitolea kwa jumuiya ya kimataifa kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi.

Alisema athari za mabadiliko ya tabia nchi huvuka mipaka na kwamba ipo haja ya hatua za dharura za kimataifa kuwanusuru wanadamu na mazingira.

Rais Ruto alisema mzozo unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi yanadhihirika kutokana na ongezeko la viwango vya joto, ukame, mafuriko na kupungua kwa kiwango cha mvua miongoni mwa majanga mengine yaliyosababisha vifo.

Alidokeza kuwa hakuna taifa linapaswa kushurutishwa kufanya maamuzi kati ya maendeleo na hatua za mabadiliko ya tabia nchi, akisema yote mawili yanaweza kutekelezwa kwa pamoja.

Alisema kuwa maamuzi ya kongamano la mwaka huu la bara Afrika kuhusu tabia nchi lililoandaliwa jijini Nairobi mwezi Septemba mwaka huu, limeliweka bara hili katika mstari wa mbele kuongoza juhudi za kuhimili athari za mabadiliko ya tabia nchi na mikakati ya kutafuta suluhu kwa bara Afrika na ulimwengu kwa jumla.

Rais Ruto aliongeza kuwa Kenya inaazimia kuhakikisha kupunguzwa kwa uzalishaji wa gesi ya kaboni kwa kutumia nishati safi.

Viongozi kadhaa duniani wanahudhuria mkutano wa COP28 jijini Dubai kubaini azima na majukumu kuhusiana na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Website | + posts