Home Habari Kuu Rais Ruto azindua ujenzi wa reli ya Riruta – Ngong

Rais Ruto azindua ujenzi wa reli ya Riruta – Ngong

Rais Ruto, aliagiza kwamba shughuli za ujenzi zikamilishwe katika muda wa miezi minane ijayo. 

0

Rais William Ruto leo Ijumaa asubuhi, alizindua ujenzi wa reli mpya ya Riruta-Ngong. 

Reli hiyo inayotarajiwa kuimarisha uchukuzi wa abiria na bidhaa katika eneo hilo, inapitia kwenye eneo la Ngong-Bulbul-Karen-Nairobi.

Akizindua ujenzi huo, kiongozi wa taifa alikariri umuhimu wa mfumo huo mpya wa uchukuzi akisema utapunguza gharama ya uchukuzi kwa wakazi wa eneo hilo kwa asilimia 50.

” Upanuzi wa huduma za reli nchini, utatoa fursa kwa Wakenya kupata mfumo nafuu na wa kutegemewa kufika kazini, kuwaunganisha watu na huduma na pia fursa za kiuchumi,” alisema Rais Ruto.

Aliagiza kwamba shughuli za ujenzi zikamilishwe katika muda wa miezi minane ijayo.

Mnamo mwezi Oktoba, shirika la reli nchini liliandikia vyama vya maeneo ya Karen na Lang’ata kuomba mashauriano na wadau kabla ya kuanza kwa mradi huo.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen na Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku, wabunge na wawakilishi wadi.