Rais William Ruto siku ya Jumatatu, aliweka jiwe la msingi katika shule ya msingi ya Kamagut alikoanzia elimu yake.
Shule hiyo inatarajiwa kufanyiwa ukarabati wa shilingi milioni 190 kwa ushirikiano baina ya serikali na wakfu wa Safaricom Mpesa.
Rais Ruto alisema madarasa tisa katika kitengo cha junior secondary pamoja na mengine kumi na mawili katika kitengo kingine cha sekondari, yatajengwa katika shule hiyo.
Ruto alizuru shule hiyo akiandamana na mama wa Taifa Rachel Ruto, waziri wa elimu Ezekiel Machogu, katibu katika wizara ya elimu Belio Kipsang pamoja na msimamizi wa wakfu wa Mpesa Michael Joseph miongoni mwa viongozi wengine.
Rais Ruto pia alitumia fursa hiyo kuahidi wananchi kuhusu kujitolea kwake kuwekeza raslimali zaidi katika elimu, akikariri kuwa walimu wana wajibu muhimu wa kutambua uwezo wa kila mwanafunzi.
Alisema serikali yake itahakikisha walimu wana nyenzo zote za kufundisha, ujuzi pamoja na usaidizi wanaohitaji ili waendelee kuboresha mustakabali wa viongozi wa siku za usoni.