Home Habari Kuu Rais Ruto awataka Wakenya kujisajili kwa hazina ya SHIF

Rais Ruto awataka Wakenya kujisajili kwa hazina ya SHIF

Rais alisema SHIF itatumia teknolojia ya hali ya juu ili kudhibiti upotevu na ufisadi.

0
Rais Ruto awataka Wakenya kujisajili kwa hazina ya bima ya afya ya SHIF.

Rais William Ruto amewataka Wakenya kujisajili kwa hazina ya Bima ya Afya ya Kijamii, (SHIF).

Rais alisema serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma wakati utekelezaji wa Mpango wa Afya kwa Wote (UHC) ukiendelea.

Katika mpango huo, alisema, watu wa kipato cha chini watachangia hadi shilingi 300 kwa mwezi, huku serikali ikiwalipia wale wasiojiweza.

Alisema SHIF itatumia teknolojia ya hali ya juu ili kudhibiti ubadhirifu na ufisadi.

“Tunaziba mianya ili kuhakikisha kuwa fedha za umma chini ya mpango huo zinatumika kutoa huduma bora za afya kwa Wakenya.”

Ruto aliongeza kuwa mkakati huo mpya utahakikisha kwamba hakuna Mkenya anayesukumwa katika umaskini kwa sababu ya bili kubwa za matibabu.

“Sasa tuna sheria inayoanzisha Hazina ya Magonjwa Sugu zaidi, ambayo itatumika kukidhi gharama za magonjwa kama saratani.  Hakuna Mkenya atakayelazimika kuuza mali yake ili kulipa bili za matibabu.”

Aliyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Kiufundi ya Belgut na Kituo cha Kidigitali cha Belgut TTI katika Kaunti ya Kericho.

Rais yuko katika ziara ya maendeleo ya kusini mwa Bonde la Ufa.