Home Biashara Rais Ruto awasili San Fransisco, Marekani kwa mkutano wa uwekezaji

Rais Ruto awasili San Fransisco, Marekani kwa mkutano wa uwekezaji

Ziara hiyo inalenga kuimarisha fursa za uwekezaji na biashara kati ya Kenya na Marekani.

0
Rais William Ruto.

Rais William Ruto amewasili katika mji wa San Fransisco ambako atahudhuria mkutano wa uwekezaji na viongozi wa kampuni za kiteknolojia nchini Marekani.

Miongoni mwa maafisa watakaokutana na Rais ni pamoja na wale wa kampuni za Apple, Intel, Microsoft, Google miongoni mwa wengine katika juhudi za kuwavutia kuwekeza nchini Kenya.

Ziara hiyo inalenga kuimarisha fursa za uwekezaji na biashara kati ya Kenya na Marekani.

Rais Ruto aliondoka humu nchini Jumatano usiku kuelekea Marekani katika ziara itakayoelezea kujitolea kwa Kenya katika uvumbuzi wa teknolojia.

Msemaji wa Ikulu ya Nairobi Hussein Mohamed, kupitia kwa taarifa alisema baadaye Rais atahudhuria mkutano wa 78 wa Umoja wa Mataifa, UN jijini New York.

“Mkutano huo utatathmini ajenda ya maendeleo ya mwaka 2030, pia utashughulikia changamoto zinazoghubika dunia kama vile janga la mabadiliko ya tabia nchi pamoja na madeni,” alisema Mohamed.

Pembezoni mwa mkutano huo wa UN, Rais Ruto pia ataongoza mkutano wa kamati ya viongozi wa nchi na serikali wa bara Afrika kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, pamoja na kushiriki majadiliano kuhusu uchumi wa baharini.