Rais William Ruto amewasili mjini Seoul nchini Korea Kusini aanakofanya ziara rasmi ya serikali.
Ameandamana na mkewe Rachel Ruto na maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini.
Punde baada ya kuwasili, Ruto alilakiwa na balozi wa Kenya nchini humo Emmy Kipsoi na Kang Seok-hee ambaye ni balozi wa zamani wa Korea Kusini nchini Ethiopia na Ushelisheli.
Rais Ruto anasema Kongamano la Korea Kusini na Afrika linatoa fursa ya kukuza uhusiano thabiti na taifa hilo la Asia kwa kutumia uimara wa Kenya kukuza ukuaji wa pande mbili, kuangazia changamoto za dunia na kuongeza umoja kwa ajili ya amani na usalama.
Ziara ya Rais Ruto nchini Korea Kusini inalenga kukamilisha kutiwa saini kwa mikataba ya maendeleo iliyoafikiwa mwezi Novemba mwaka jana, alipozuru taifa hilo la bara Asia.
Baadhi ya maafikiano ya mwaka jana ilikuwa serikali ya Korea Kusini kutoa shilingi bilioni 40 kwa sekta ya uchumi bunifu na mitambo ya kujenga mabwawa ya unyunyuziaji maji mashamba ya thamani ya shilingi bilioni 25.
Kwenye ziara hiyo, Rais atakutana na mwenyeji wake Yoon Suk Yeol.