Rais William Ruto ametoa wito kwa wawekezaji nchini China kuwazia kutumia nafasi zilizopo katika nyanja za nishati, maji na nyumba kuwekeza nchini Kenya.
Amesema Kenya itawaunga mkono wawekezaji wa kigeni wanaoweza kujihusisha na uongezaji thamani wa malighafi tele yaliyopo nchini humo, hususan katika sekta za nishati, maji na nyumba.
“Tuna fursa nyingi mnazoweza kuwekeza hasa katika nyanja za nishati, maji na nyumba,” alisema Rais Ruto aliyeanza ziara ya siku tatu nchini China jana Jumapili.
Aliyasema hayo leo Jumatatu wakati akizuru kampuni ya uhandisi ya Engineering Corporation Limited jijini Beijing.
Kampuni hiyo hujihusisha na utoaji suluhu za pamoja za nishati, ujenzi, vifaa na utengenezaji bidhaa miongoni mwa shughuli zingine.
Wakati wa ziara hiyo, Rais Ruto alishuhudia utiaji saini wa Mkataba wa Maelewano kati ya Wizara ya Nishati na Energy China.