Rais William Ruto amewataka maafisa wa usalama wanaojihusisha na biashara ya pombe kukoma mara moja au wasimamishwe kazi.
Akihutubia wakazi wa kaunti ya Kericho, Ruto alikariri kuwa serikali yake haitamsaza yeyote na kwamba itafanya juu chini kutokomeza biashara hiyo ambayo imeharibu maisha ya vijana wengi nchini.
Rais pia alisema kuwa mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu ni mojawapo wa ajenda kuu za serikali na ni sharti utaendelea, akiutaja kuwa wenye manufaa mengi na tayari umetoa nafasi nyingi za ajira kwa vijana.
Aidha, Rais aliwashukuru wakulima wa Kericho kwa kuchangia kushuka kwa gharama ya bei ya vyakula kama vile unga wa mahindi.
Rais ambaye aliandamana na Naibu wake Rigathi Gachagua na viongozi wa eneo hilo, amefichua kwamba serikali imetenga shilingi bilioni moja za kusambaza umeme kwa wakazi wa eneo hilo kupitia mpango wa ‘Last Mile’.
Kwa upande wake, Gachagua amemtataka mkandarasi anayejenga nyumba za bei nafuu eneo hilo kuwapa vijana na kina mama kipaumbele wakati wakuwaajiri wafanyakazi.
Rais yuko kwenye ziara ya siku mbili kusini mwa Bonde la Ufa na pia amezindua miradi kadhaa ikiwemo kituo cha uchapishaji wa pasipoti.