Home Habari Kuu Rais Ruto awaomboleza maafisa wa KDF walioangamia katika ajali ya helikopta

Rais Ruto awaomboleza maafisa wa KDF walioangamia katika ajali ya helikopta

0
Rais William Ruto

Rais William Ruto amepeleka risala za rambirambi kwa ndugu na marafiki wa maafisa wa vikosi vya ulinzi nchini walioaga dunia kufuatia ajali ya ndege ya helikopta katika kaunti ya Lamu.

Kwenye taarifa Rais Ruto alisema kuwa nchi hii inaheshimu ushujaa wao katika kulinda na kuhifadhi uhuru wa nchi hii.

Alikifariji kikosi kizima na wale wote walioathiriwa na mkasa huo. Vikosi vya KDF vimebuni bodi ya kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.

“Tunaheshimu ujasiri wao katika kulinda taifa hili. Tunaombea kikosi kizima cha KDF na wale wote walioadhiriwa na ajali hiyo,” alisema Rais kupitia mtandao wa twitter.

Idara ya ulinzi kwenye taarifa ilisema kuwa ndege hiyo ya helikopta ya kijeshi aina ya Huey ilianguka wakati wa doria za usiku katika kaunti ya Lamu, ambayo katika siku za hivi maajuzi imeshuhudia ongezeko la mashambulizi ya kigaidi.

Ilisema kuwa wahudumu na maafisa wa kijeshi waliokuwa ndani walikuwa sehemu ya kundi la uchunguzi wa angani linaloimarisha doria wakati wa mchana na usiku na uchunguzi kuhusiana na operesheni inayoendelea ya Amani Boni.

Ingawa idara hiyo haikubainisha idadi kamili ya waathiriwa ilipeleka risala za rambirambi kwa familia za wanajeshi walioaga dunia kwenye ajali hiyo.

Radio Taifa
+ posts