Home Habari Kuu Rais Ruto awakaribisha wawekezaji wa Marekani nchini Kenya

Rais Ruto awakaribisha wawekezaji wa Marekani nchini Kenya

Rais alisema Kenya ina mazingira bora ya uwekezaji katika teknolojia na uzalishaji bidhaa.

0
Rais Ruto akaribisha wawekezaji wa Marekani nchini Kenya.

Rais William Ruto amealika kampuni za Marekani za teknolojia kuanzisha shughuli za uzalishaji bidhaa na kufungua afisi za kanda nchini Kenya.

Rais alisema Kenya ina mazingira bora ya uwekezaji katika teknolojia na uzalishaji bidhaa.

“Kenya ni kitovu cha uwekezaji, ina uchumi dhabiti, ni salama, ina mazingira bora ya ulipaji ushuru, ina wafanyikazi walio na ujuzi na kebo za majini zinazohakikisha uunganishwaji mtandao wa kutegemewa,”alisema Rais.

Kiongozi wa taifa aliyasema hayo alipokutana na maafisa wakuu wa kampuni ya Apple Tim Cook, Patrick Gelsinger wa Intel,  Ruth Porat wa Google, Brad Smith wa Microsoft pamoja na wengine wa Nike, GAP na Levi Strauss, jijini  San Francisco nchini Marekani.

Aidha aliwahakikishia wawekezaji hao kuwa serikali itazingatia na kushughulikia masuala  ibuka, ili kuimarisha imani yao humu nchini.

Kampuni hizo za Marekani zilionyesha imani kwa Kenya kuwa eneo bora la uwekezaji.

Afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Apple Tim Cook, alisema kampuni ya Apple itawekeza katika mfumo wa data wa Kenya.

Kwa upande wake afisa mtendaji wa kampuni ya Intel Patrick  Gelsinger, alisema kwa mtazamo wake, Kenya ni kituo muhimu cha uwekezaji.

Ruth Porat wa kampuni ya Google alisema kampuni yake itawekeza dola bilioni moja za Marekani, kuimarisha utoaji mafunzo ya kidijitali na mikakati ya uvumbuzi.

Website | + posts