Home Kimataifa Rais Ruto awahimiza Wakenya kudumisha amani

Rais Ruto awahimiza Wakenya kudumisha amani

Aliwatahadharisha Wakenya dhidi ya ghasia, uharibifu wa mali, uporaji na vitendo vinavyosababisha kupoteza maisha.

0
Rais William Ruto akiwahutubia wananchi.
kra

Rais William Ruto amesema uamuzi wake wa kuunda serikali ya muungano, unalenga kuwaleta pamoja Wakenya kutoka sehemu zote za jamii kuunga mkono ajenda ya mabadiliko nchini.

Akizungumza leo Alhamisi katika ziara ya ukaguzi wa mipango ya maendeleo katika Kaunti ya Tharaka Nithi, Rais alisema serikali iliyojumuisha wote haitamwacha mtu nyuma.

kra

Alidokeza kwamba maendeleo hayatakuwa rahisi ikiwa hakutakuwa na umoja na ushirikiano kati ya Wakenya.

“Kwa sababu ya changamoto zinazotukabili, nimeamua kuunda serikali ya muungano ambayo itahusisha mikoa yote,” alisema Rais katika mji wa Marimanti.

Rais Ruto alitoa wito kwa Wakenya kuachana na vitendo vinavyoweza kuharibu nchi na kuyumbisha ajenda yake ya maendeleo.

Aliwatahadharisha Wakenya dhidi ya ghasia, uharibifu wa mali, uporaji na vitendo vinavyosababisha kupoteza maisha.

“Hatuna nchi nyingine.  Tunayo hii tu.  Mkiiharibu hii, hatutakuwa na pa kwenda.”

Rais Ruto alisema serikali inaangazia kuzindua mipango ambayo itabadilisha maisha ya Wakenya na kuipeleka nchi katika ngazi ya juu zaidi.

Alieleza kuwa serikali inazindua mpango wa Huduma ya Afya kwa Wote, UHC ili kurahisisha Wakenya kupata huduma bora za afya na za bei nafuu.

“Huduma ya Afya kwa Wote ambayo tumekuwa tukiijadili kwa miaka mingi inatekelezwa.  Tumebadilisha sheria na tuna vipande vinne vya sheria ili kuhakikisha inatimika,” Rais alisema.

Alibainisha kuwa ujenzi na utayarishaji wa Vyuo vya Mafunzo ya Tiba vya Kenya kote nchini utaimarisha uwezo wa wahudumu wa afya na kuimarisha utekelezaji wa Huduma ya Afya kwa Wote.

Rais Ruto alidokeza kuwa Mpango wa Serikali wa Nyumba za Gharama Nafuu umebuni nafasi za kazi 160,000 kwa vijana, akisema mpango huo ni kuongeza miradi na kubuni nafasi zaidi za kazi.

Alisema serikali inajenga masoko 400 ya mazao mapya kote nchini Kenya, akiongeza kuwa katika Kaunti ya Tharaka Nithi, yatajengwa Marimanti, Ciakariga na Gaatunga ili kuhakikisha wafanyabiashara wana maeneo ya kufanyia kazi yanayostahili.

Kwa upande wake, Bw Gachagua alisema serikali imejitolea kubadilisha kaunti hiyo, ambayo alibaini kuwa iko nyuma.

Alisema watamuunga mkono Rais Ruto ili kutimiza ajenda ya maendeleo ya nchi.

Aliandamana na Naibu wake Rigathi Gachagua, Gavana wa Tharaka Nithi Muthomi Njuki, wabunge na Wawakilishi wa Wadi kadhaa.