Home Habari Kuu Rais Ruto atua Nyanza kwa ziara ya kimaendeleo

Rais Ruto atua Nyanza kwa ziara ya kimaendeleo

Kiongozi wa taifa atazuru kaunti za Kisumu, Homa Bay, Siaya na Migori.

0
Rais William Ruto.

Rais William Ruto leo Ijumaa anaanza ziara ya siku nne katika eneo la Nyanza, ambako atazindua miradi ya maendeleo katika eneo hilo.

Kiongozi wa taifa atazuru kaunti za Kisumu, Homa Bay, Siaya na Migori.

Miradi itakayozinduliwa inalenga kuimarisha maisha ya wakazi wa eneo hilo, kupitia kupunguza gharama ya maisha, kubuni nafasi za ajira, pamoja na kustawisha sekta za kilimo, afya, biashara ndogo na za kadri, miongoni mwa sekta zingine.

Katika kaunti ya Kisumu, Rais Ruto atazindua ujenzi wa mradi wa kituo cha kufuga samaki cha Kabonyo cha thamani ya shilingi bilioni moja. Uzinduzi wa mradi huo unalenga kufufua uchumi wa baharini katika eneo la ziwa Victoria.

Rais pia atazindua kituo cha kibiashara cha Lake Basin Mall, ambacho kinatarajiwa kuinua biashara, uchumi na ukuaji wa mji wa Kisumu na viunga vyake.

Aidha Rais atazindua meli ya MV Uhuru 2 ambayo itafanikisha uchukuzi wa watu na bidhaa katika ziwa Victoria.

Siku ya Alhamisi, waziri wa habari mawasiliano na uchumi wa kidijitali Eliud Owalo,  alitaja ziara hiyo ya Rais kuwa ya kihistoria katika eneo hilo, alilotaja limesalia nyuma kimaendeleo kwa miaka mingi.

Owalo alisema Rais atakamilisha ziara yake kwa kuandaa mkutano wa baraza la mawaziri katika ikulu ndogo ya kisumu siku ya Jumatatu.

Aliwasihi wakazi wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi kumkaribisha kiongozi wa taifa, akisema kuwa tangu taifa hili kupata uhuru, hakuna miradi ya maendeleo ya aina hiyo imewahi kuzinduliwa katika eneo hilo.

Website | + posts