Home Habari Kuu Rais Ruto atetea mradi wa nyumba za gharama nafuu

Rais Ruto atetea mradi wa nyumba za gharama nafuu

0

Kiongozi wa nchi Rais William Ruto kwa mara nyingine ametetea mradi wa nyumba za gharama nafuu akitaja utoaji wa nafasi za ajira kama sehemu ya mazuri yanayotokana nao.

Akizungumza katika uwanja wa michezo wa Ulinzi wakati wa hafla ya kusherehekea miaka 100 ya kanisa la Salvation Army, kiongozi wa nchi alisema mradi huo pia utahakikishia wakenya makazi mazuri.

Rais Ruto alisisitiza kwamba serikali yake imejitolea kikamilifu katika kutekeleza mpango ambao utasaidia wakenya kujikimu hasa wale wa mapato ya chini.

Alisema wakenya wengi wanaoishi kwenye mitaa ya mabanda wanastahili kupata makazi mazuri na ni jukumu la walio na ajira kuchanga fedha za kufanikisha hilo.

Ruto alisema pia kwamba serikali yake inataka kutoa ajira kwa vijana kupitia mradi wa nyumba za bei nafuu, kuwapeleka ughaibuni kwa kazi, kuhakikisha wanapata ajira mitandaoni na kuajiriwa katika viwanda.

Kiongozi huyo alishukuru viongozi na waumini wa kanisa la Salvation Army kwa mipango ambayo kanisa hilo limekuwa likitekeleza katika jamii huku akiwataja kuwa kielelezo.

Aligusia hasa usaidizi unaotoka kwa kanisa hilo kwa wasiobahatika katika jamii hasa walemavu akisema wote watabarikiwa na Mungu ambaye pia atawawezesha kuendeleza huduma.

Rais alihakikishia kanisa la Salvation Army uungwaji mkono kutoka kwa serikali na kuahidi kwamba serikali itashirikiana na kanisa hilo kuendeleza huduma kwa wakenya.

Kanisa la Salvation Army lilianzishwa nchini Kenya mwaka 1923 na sherehe hizo ambazo zilifanyika kwa siku tatu kuanzia Ijumaa ziliongozwa na kiongozi wa Salvation Army ulimwenguni General Lyndon Buckingham na kiongozi wa kanisa hilo nchini Kenya Colonel Daniel Kiama.

Website | + posts