Rais William Ruto ametajwa na Jarida la Time Magazine, kuwa mmoja wa viongozi 100 wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani wanaochagia mabadiliko ya tabianchi duniani.
Uorodheshaji huo unajiri katika wiki ambayo aliongoza likizo ya kitaifa iliyolenga kupanda miti milioni 100 kwa siku moja.
Ruto alitajwa pamoja na meya wa mji mkuu wa Sierra Leone Freetown, Yvonne Aki-Sawyerr.Msanifu wa Burkinabe-Ujerumani Francis Kéré na mjasiriamali wa hali ya hewa wa Ethiopia Kidus Asfaw ni miongoni ya walioorodheshwa
Orodha hiyo, inayojulikana kama “Time 100 Climate”, ilitolewa Alhamisi, na ni jaribio la uzinduzi wa jarida hilo kutaja wale inaowaona kuwa muhimu katika kuangazia na kufanya kitu kuhusu suala la mabadiliko ya hali ya hewa kote ulimwenguni.
Time Magazine ilisema ilichagua wale walioorodheshwa kwa “kufanya maendeleo makubwa katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi “.
Jarida hilo pia lilisema kuwa washindi hao walichaguliwa kwa sababu ya juhudi zao katika kupambana na mabadiliko ya hali ya anga
Rais Ruto amekuwa na sauti katika kujaribu kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa nchini Kenya na Afrika.
Likizo ya upandaji miti iliyofanyika tarehe 13 Novemba ilikuwa sehemu ya azma yake kubwa kwa Kenya kupanda miti bilioni 15 katika miaka 10.
Mnamo Septemba, aliandaa Mkutano wa kwanza kabisa wa hali ya hewa barani Afrika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ambao ulimalizika kwa tamko la pamoja la kutaka wachafuzi wa mazingira watoe rasilimali zaidi kusaidia mataifa maskini.
Lakini baadhi ya wanamazingira wamemtaja Ruto kuwa mnafiki kwa kutetea upandaji miti huku akikosa kudhibiti ukataji miti ovyo katika misitu ya umma.
Mwezi uliopita, mahakama ya mazingira ilisitisha agizo ambalo Rais Ruto alitoa mnamo Juni kuondoa marufuku ya 2018 ya ukataji miti.