Home Habari Kuu Rais Ruto ashinikiza kuhusishwa kwa wasio na ajira katika mazungumzo ya ILO

Rais Ruto ashinikiza kuhusishwa kwa wasio na ajira katika mazungumzo ya ILO

Hii, alielezea itafungua njia kwa ajili ya ufumbuzi endelevu wa ukosefu wa ajira.

0

Rais William Ruto amelitaka Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) kupanua mazungumzo yake na kuwajumuisha wasio kuwa na ajira.

Alisema mfumo wa ILO umekuwa ukiegemea zaidi wafanyakazi lakini haki za kazi pia zinawagusa wasio kuwa na ajira.

Hii, alielezea itafungua njia kwa ajili ya ufumbuzi endelevu wa ukosefu wa ajira.

“Tunapozungumzia mambo yanayohusu kazi, lazima pia tuzungumze kuhusu mamilioni ya watu wasio kuwa na kazi ambao sauti zao haziwezi kusikika katika mikutano kama hii,” alisema.

Rais Ruto aliyasema hayo siku ya Alhamisi wakati wa Kongamano la Kimataifa la Kazi Duniani la ILO mjini Geneva, Uswizi.

Rais alisema inasikitisha kwamba Afrika imerekodi viwango vya juu zaidi vya ukosefu wa ajira duniani huku nchi nyingi zikiripoti kati ya robo na theluthi ya watu wao kuwa wasio na kazi.

Alitoa wito kwa Mataifa ya Afrika kuharakisha utekelezaji wa Ajenda 2063 na malengo ya maendeleo endelevu ili kubuni fursa zaidi kwa watu.

Rais Ruto alisema kuimarisha soko la Afrika kupitia utekelezaji wa Eneo Huria la Biashara barani Afrika kutaleta nafasi zaidi za kazi.

“Afrika ina fursa kubwa ya kubadilisha kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa kiuchumi, na hivyo kutengeneza ajira kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea,” alisema.

 

Website | + posts

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here