Home Taifa Rais Ruto asema uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni kinyume cha sheria

Rais Ruto asema uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni kinyume cha sheria

0
kra

Rais William Ruto amesema kwamba uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni kinyume cha sheria, hatua isiyokuwa ya haki na ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Rais Ruto anasema kwamba wakati umewadia kwa wahusika wa vita hivyo kudhihirisha imani na kuacha misimamo mikali ili kuafikia amani ya kudumu.

kra

“Tunapoanzisha juhudi za pamoja za kutatua mzozo wa Ukraine na mizozo mingine ulimwenguni, wakati umewadia kwa wahusika wa vita hivi kuonyesha imani na kuacha kuwa na misimamo mikali ili kuafikia amani ya kudumu.” alisema Rais Ruto.

Kiongozi wa nchi ameungana na viongozi wengine wa ulimwengi kwa kongamano kuhusu amani nchini Ukraine ambalo linafanyika katika hoteli ya Bürgenstock nchini Switzerland.

Katika hotuba yake, Rais Ruto alisema kwamba huo ndio msimamo wa Kenya kuhusu vita vya Ukraine kwani Kenya inazingatia sheria ya kimataifa ambayo inahimiza usawa na uhuru wa mataifa mbali mbali, kuheshimu mipaka ya himaya za nchi mbali mbali na kusuluhishwa kwa mizozo kwa njia ya amani.

Alisema pia kwamba vita hivyo vya Ukraine na mizozo mingine ulimwenguni ikiwemo ya bara Afrika imeathiri kila mmoja. Alisema mizozo hiyo imesababisha athari kama ukosefu wa chakula cha kutosha.

“Katika eneo la magharibi mwa Afrika, shule ambazo zimefungwa zimefikia 13,250, na hivyo kunyima watoto wengi fursa ya kupata elimu. Kufikia Juni, 2023, shule za msingi 7,800 ambazo zilikuwa zinahudumia jumla ya wanafunzi milioni 1.4 zilifungwa katika eneo la Sahel.” alisema rais Ruto huku akihimiza utatuzi wa mizozo haraka.

Akihutubia kongamano hilo, kiongozi wa taifa la Ukraine Volodymyr Zelensky alisema kwamba kando na kutafuta amani ya kudumu katika nchi yake, kongamano hilo linaonyesha pia kwamba juhudi za pamoja zinaweza kukomesha vita na kuleta amani.

Hata hivyo Zelensky alilalamikia kutokuwepo kwa wawakilishi wa Urusi katika kongamano hilo akisema kwamba taifa hilo halitaki amani kwani lingetaka amani lingejumuika na mataifa mengine kwenye kongamano hilo.

Huku kongamano hilo likiendelea, vita vinaendelea pia nchini Ukraine ambapo mashambulizi ya Urusi yalisababisha vifo vya raia watatu na wengine 15 wakajeruhiwa Ijumaa jioni mpaka Jumamosi asubuhi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here