Home Habari Kuu Rais Ruto asema ujenzi wa nyumba za bei nafuu unaendelea vyema

Rais Ruto asema ujenzi wa nyumba za bei nafuu unaendelea vyema

0

Kiongozi wa nchi William Ruto amesema kwamba ujenzi wa nyumba 46,792 unaendelea katika sehemu mbali mbali za nchi huku ujenzi wa nyingine elfu 40 ukikaribia kuanza.

Aliyasema hayo wakati wa hotuba yake bungeni kuhusu hali ya nchi hii ambapo alielezea pia kwamba mpango huo wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu umesababisha upatikanaji wa nafasi za ajira elfu 50.

Kulingana naye, idadi ya nafasi za ajira itaongezeka zaidi awamu nyingine za ujenzi wa nyumba hizo zitakapoanza.

“Jumla ya nyumba 746,795 zinatarajiwa kujengwa nchini zikiwa katika viwango tofauti tofauti vya utekelezaji.” alisema Rais Ruto.

Huku akikiri kwamba tatizo la nyumba za makazi linahisiwa sana mijini na sio vijijini, kiongozi wa nchi alisema kwamba tatizo hilo linasababisha hofu kubwa kiafya na kiusalama pamoja na kushusha hadhi ya watu hasa wa mapato ya chini.

Alisema ukosefu wa nyumba za bei nafuu unasababisha ujio wa mitaa ya mabanda na ni lazima mpango wa nyumba za gharama nafuu uharakishwe ili kutatua suala hilo.

Kulingana naye kuna nyumba aina tatu chini ya mpango huo za kijamii, za gharama nafuu na zitakazouzwa kwa bei ya kawaida.

Riba za mikopo ya kununua nyumba hizo alisema zitakuwa za chini mno yaani tarakimu moja. Katika nyumba za makazi ya kijamii riba itakuwa asilimia 3, nyumba za gharama nafuu asilimia 6 na nyumba za bei ya kawaida riba itakuwa asilimia 9.

Alishukuru serikali za kaunti kwa kuunga mkono ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.

Kando na nyumba za makazi Rais alisema serikali inajenga masoko 400 katika sehemu mbali mbali za nchi ili kina mama wapate mahali pazuri pa kuuzia bidhaa zao.

Website | + posts