Home Habari Kuu Rais Ruto asema safari zake ni za kufaidi Kenya

Rais Ruto asema safari zake ni za kufaidi Kenya

0

Rais William Ruto ametetea safari zake nje ya nchi ambazo zimekuwa mada kwenye vinywa vya wakenya kadhaa.

Akizungumza jana Jumapili wakati wa ibada katika kaunti ya Kiambu, Rais Ruto alisema kwamba ziara ambazo amekuwa akifanya kwenye nchi nyingine zinalenga kunufaisha Kenya hasa katika ukuaji na wala sio za kujifurahisha.

Kiongozi wa nchi alisema kwamba ziara hizo huwa anazifanya kwa mpango na kwamba yeye sio mtalii akiongeza kwamba Kenya inahitaji mabadiliko ambayo yataafikiwa tu kupitia mawazo mazuri na mipango.

Alisema kwamba waziri wa Leba Florence Bore yuko Saudi Arabia kwa sababu ya mipango ya vijana wa Kenya kupata ajira huko.

Makubaliano yaliyoafikiwa kwenye ziara zake, rais Ruto alisema yatafanya vijana wengi kusafiri nje ya nchi hivi karibuni kwa sababu ya upatikanaji wa fursa za ajira katika nchi mbali mbali.

Anasema hiyo ni sehemu ya suluhisho kwa tatizo lililokithiri la ukosefu wa ajira humu nchini.