Home Habari Kuu Rais Ruto asema hatua mwafaka zimechukuliwa kuimarisha uchumi

Rais Ruto asema hatua mwafaka zimechukuliwa kuimarisha uchumi

0

Rais William Ruto amesema kwamba serikali imechukua hatua stahiki za kushughulikia mkwamo wa kiuchumi na sasa iko mahali salama kuweza kuwajibikia madeni yake.

Alisema hatua hizo ni pamoja na kupunguza matumizi ya fedha ili kupunguza kukopa na kuzinduliwa kwa masharti mapya ya ushuru ili kuongeza kiwango cha mapato yanayokusanywa.

Rais alisema pia kwamba kuondolewa kwa ruzuku kulichochea ongezeko la uzalishaji wa chakula kwa asilimia 40 kwa gharama ya chini ikilinganishwa na gharama ya awali huku wakenya wengi wakipata nafasi za ajira na biashara.

Katika hotuba yake ya kukaribisha mwaka mpya aliyotoa katika ikulu ya Nakuru, Rais Ruto alikiri kwamba alifanya maamuzi fulani ya kuumiza lakini yenye manufaa ya baadaye.

Kiongozi wa taifa alikubali kwamba nchi imepitia changamoto nyingi zilizotokana na mabadiliko ya tabianchi na vita nchini Ukraine lakini ana imani kwamba mwaka huu wa 2024 mambo yatakuwa sawa.

Rais William Ruto aliandaa hafla ya chakula cha jioni ambayo pia ilikuwa ya kukaribisha mwaka mpya na ilihudhuriwa na viongozi wakuu serikalini na viongozi wa kidini.

Website | + posts