Home Kimataifa Rais Ruto asema Afrika imejitambulisha katika suala la mabadiliko ya tabianchi

Rais Ruto asema Afrika imejitambulisha katika suala la mabadiliko ya tabianchi

0

Rais wa Kenya William Ruto amesema kwamba katika muda wa mwaka mmoja uliopita Afrika imejitambulisha vilivyo katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Kulingana naye utambulisho huo ni katika kanda hii na katika ulimwengu mzima na kwamba uathirika uliotumiwa na bara hili awali katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi sasa umebadilika na kuwa mjadala imara kuhusu jukumu la bara hili.

Alisema katika kongamano la kwanza la mabadiliko ya tabianchi barani Afrika jijini Nairobi, Septemba mwaka jana, bara liliafikia mapendekezo kadhaa.

Yanajumuisha jinsi ulimwengu unaweza kutumia raslimali za kiasili za Afrika kuondoa gesi ya Carbon huku misitu ya bara hili ikitumiwa kama maeneo ya kufyonza gesi hiyo.

“Kupitia hifadhi kubwa ya kawi safi ya bara Afrika, bara hili limekuwa wazi kuhusu jinsi eneo la kaskazini la ulimwengu linaweza kubadili utengenezaji bidhaa na shughuli za viwanda.” alisema Rais.

Rais Ruto anasema hatimaye hilo litaimarisha utengenezaji bidhaa barani Afrika na kutoa fursa za ajira kwa vijana wengi.

Aliyasema haya alipokuwa akiongoza kikao cha kamati ya Marais na viongozi wa serikali za bara Afrika kuhusu mabadiliko ya tabianchi katika makao makuu ya Umoja wa Afrika jijini Addis Ababa, nchini Ethiopia.

Viongozi waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Rais Azali Assoumani wa Comoros, wa Zambia Hakienda Hichilema, Naibu Rais wa Ushelisheli Ahmed Afif, waziri wa mazingira wa Kenya Soipan Tuya, Mkurugenzi mkuu wa UNEP Inger Andersen na kamishna wa Umoja wa Afrika kuhusu mazingira Josefa Sacko.

Website | + posts