Home Taifa Rais Ruto arejea nchini baada ya ziara nchini Italia na Uswizi

Rais Ruto arejea nchini baada ya ziara nchini Italia na Uswizi

0
kra

Rais William Ruto amerejea nchini kutoka mataifa ya Italia na Uswizi ambako alihudhuria mkutano wa mataifa 7 yenye ustawi mkubwa kiviwanda duniani, G7 na kongamano la amani nchini Ukraine mtawalia.

Rais alilakiwa katika uwanja wa ndege na viongozi wakuu serikalini akiwemo Waziri wa Usalama wa Taifa Kithure Kindiki, kiongozi wa wengi bungeni Kimani Ichung’wah, Seneta Aaron Cheruiyot na wengine.

kra

Katika mkutano wa G7 jijini Apulia nchini Italia, Rais Ruto aliwataka viongozi wa ulimwengu kuungana katika kukabili changamoto zinazokumba ulimwengu.

Aliwahakikishia kwamba bara la Afrika liko tayari kutekeleza wajibu wake kikamilifu na ndiyo sababu Umoja wa Afrika, AU unapanga mabadiliko ya kimkakati ili kuufanya kuwa shirika muhimu litakalotambuliwa na kuhusishwa katika mazungumzo kuhusu changamoto mbalimbali ulimwenguni ili kuhakikisha ufanisi wa pamoja.

Alipohutubia kongamano la amani nchini Ukraine huko Bürgenstock, nchini Uswizi, Ruto alisema uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ni kinyume cha sheria, hatua isiyokuwa ya haki na ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Alisema wakati umewadia kwa wahusika wa vita hivyo kudhihirisha imani na kuacha misimamo mikali ili kuafikia amani ya kudumu.

Rais Ruto aliongeza kwamba huo ndio msimamo wa Kenya kuhusu vita vya Ukraine kwani Kenya inazingatia sheria ya kimataifa ambayo inahimiza usawa na uhuru wa mataifa mbalimbali, kuheshimu mipaka ya himaya za nchi mbalimbali na kusuluhishwa kwa mizozo kwa njia ya amani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here