Home Habari Kuu Rais Ruto aongoza jumbe za maombolezi ya Kelvin Kiptum

Rais Ruto aongoza jumbe za maombolezi ya Kelvin Kiptum

0

Viongozi katika nyanja mbalimbali na wanamichezo wakiongozwa na Rais William Ruto wanaendelea kumwomboleza mwanariadha mashuhuri Kelvin Kiptum.

Kupitia taarifa, Rais Ruto amemtaja marehemu Kiptum kuwa nyota na mmoja wa wanamichezo waliokiuka vikwazo mbalimbali na kuibuka washindi, washikilizi wa rekodi za mbio za marathon.

“Ushupavu wake kiakili na nidhamu ni vya kupigiwa mfano. Kiptum alikuwa mustakabali wetu. Mwanamichezo wa kipekee ameacha alama ya kuenziwa ulimwenguni,” alisema Rais Ruto.

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa upande wake anasema nchi ya Kenya imepoteza shujaa wa kweli huku akitoa salamu za pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wadau wote wa riadha.

“Ni taarifa za kusikitisha tunapoomboleza kifo cha mtu wa kipekee, Kelvin Kiptum, mshikilizi wa rekodi ya dunia na bingwa wa riadha nchini Kenya,” alisema Raila kwenye taarifa.

Mwanamichezo David Rudisha alisema vifo vya Kiptum na kocha wake Gervais Hakizimana, vimemshtua na kumhuzunisha sana.

Rudisha alitoa risala za rambirambi kwa familia na marafiki wa wawili hao na jamii nzima ya wanariadha nchini Kenya akitaja vifo hivyo kuwa hasara kubwa.

Kelvin Kiptum na Kocha wake Gervais Hakizimana kutoka Rwanda waliangamia usiku wa Jumapili, Februari 11, 2024 kwenye ajali ya barabarani katika eneo la Eldoret-Kaptagat.

Website | + posts