Home Habari Kuu Rais Ruto amuomboleza hayati Rais mstaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi

Rais Ruto amuomboleza hayati Rais mstaafu wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi

Rais William Ruto alisema hayati Mwinyi alikuwa kiongozi shupavu.

0
Hayati Ali Hassan Mwinyi.

Rais William Ruto ameomboleza kifo cha aliyekuwa rais wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi. Rais Samia Suluhu wa nchi hiyo alitangaza kifo cha Mwinyi Alhamisi usiku.

Kwenye taarifa kupitia mtandao wa X, rais Ruto alisema hayati Mwinyi alikuwa kiongozi shupavu.

“Natuma risala za rambi rambi kwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu na raia wa Tanzania, kufuatia kuaga dunia kwa Rais wa pili wa taifa hilo Ali Hassan Mwinyi. Tunaungana katika kuomboleza kifo cha kiongozi huyo shupavu. Lala salama Mzee Mwinyi,” alisema Rais Ruto.

Mwinyi aliyekuwa rais wa pili ya Tanzania kati ya mwaka wa 1985 na 1995, alilazwa hospitalini mapema mwezi jana huku familia ikisema alikuwa akipokea matibabu ya kifua.

Rais huyo wa zamanai alifariki kutokana na maradhi ya saratani.

Rais Suluhu alitangaza kwamba hayati Mwinyi atazikwa tarehe mbili mwezi huu katika eneo la Ugunja kwenye kisiwa cha Zanzibar.

Rais Suluhu pia alitangaza muda wa maombolezi ya kitaifa wa siku saba ambapo bendera zote nchini humo zitapeperushwa nusu mlingoti.

Mwinyi alichukua hatamu za uongozi baada ya kiongozi mwanzilishi wa taifa hilo hayati Julius Nyerere.

Kabla ya kuwa rais, Mwinyi alihudumu kwenye nyadhifa tofauti serikalini ikiwemo waziri wa usalama wa kitaifa na makamu wa rais.Mwinyi pia aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa chama tawala cha CCM kutoka mwaka 1990 hadi 1996.

Baada ya kustaafu hayati Ali Hassan Mwinyi hakujihusisha tena na maswala ya umma lakini aliendelea kuishi mjini Dar es Salaam. Mwanawe wa kiume Dr Hussein Ali Mwinyi, ndiye rais wa sasa wa kisiwa cha Zanzibar.

Website | + posts