Home Habari Kuu Rais Ruto alifanyia Baraza la Mawaziri mabadiliko

Rais Ruto alifanyia Baraza la Mawaziri mabadiliko

0

Baraza la Mawaziri limefanyiwa mabadiliko katika hatua inayolenga kuboresha utendakazi serikalini kwa mujibu wa Ajenda ya Mabadiliko ya Kiuchumi kuanzia Chini hadi Juu, BETA.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais William Ruto kulifanyia mabadiliko baraza hilo tangu aliposhika hatamu za uongozi wa taifa.

Katika mabadiliko hayo, Musalia Mudavadi ameongezwa mamlaka na sasa atahudumu kama Waziri Mwenye Mamlaka Makuu na pia Waziri wa Mambo ya Nje.

Kabla ya mabadiliko hayo, Dkt. Alfred Mutua alihudumu kama Waziri wa Mambo ya Nje.

Dkt. Mutua sasa atahudumu kama Waziri wa Utalii na Wanyama Pori, wadhifa ambao ulishikiliwa na Peninah Malonza.

Malonza sasa ametwikwa jukumu la kuongoza Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Maeneo Kame na Maendeleo ya Kikanda ambayo awali ilishikiliwa na Rebeccah Miano.

Miano sasa anarithi wadhifa ulioshikiliwa na Moses Kuria wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda.

Kuria ambaye amekuwa akishtumiwa mara kwa mara kutokana na semi zake tatanishi sasa amehamishiwa Wizara ya Utumishi wa Umma, Utendakazi na Usimamizi wa Utoaji Huduma ambayo awali ilishikiliwa na Aisha Jumwa ingawa imefanyiwa mabadiliko kidogo.

Jumwa sasa atahudumu kama Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi.

Waziri wa Maji Alice Wahome ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akilumbana na Katibu katika wizara hiyo pia amehamishwa katika mabadiliko hayo.

Wahome sasa ameteuliwa kuhudumu kama Waziri wa Ardhi, Ujenzi, Nyumba na Ustawi wa Miji akibadilishana na Zacharia Njeru ambaye amateuliwa kumrithi katika Wizara ya Maji, Usafi na Unyunyiziaji Maji Mashamba.

Website | + posts