Home Habari Kuu Ruto akubali mpango wa Biden wa kusitisha vita Gaza

Ruto akubali mpango wa Biden wa kusitisha vita Gaza

0
Rais William Ruto aongoza sherehe za Madaraka katika kaunti ya Bungoma.

Rais William Ruto ametangaza kwamba anakubaliana na mpango wa Rais wa Marekani Joe Biden wa kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza.

Kupitia taarifa kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, Ruto alifafanua kuhusu mpango huo wa Marekani wa kusitisha alichokitaja kuwa mgogoro unaozidi kuchacha kati ya Israel na Palestina.

Mpango huo uliobuniwa na Marekani, Qatar na Misri, unahusisha kusitisha vita kwa wiki sita, kuondolewa kwa wanajeshi wa Israel katika sehemu zenye watu wengi huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka.

Rais Ruto anahisi kwamba mpango huo ukitekelezwa kikamilifu, utatoa fursa ya mpango wa kujenga upya Gaza.

Amewataka wahusika wote kukubali mpango huo kama njia ya kusitisha mateso ambayo wakazi wa Gaza wamepitia tangu vita vilipoanza Oktoba 7, 2023.

“Ninaamini kwamba huu mpango ukiungwa mkono na kutekelezwa kikamilifu, utakuwa msingi wa kusitishwa kabisa kwa vita,” alisema Rais kwenye taarifa yake.

Aliongeza kwamba utasaidia katika kuafikiwa kwa suluhisho la nchi mbili za Israel na Palestina ambapo zitakubaliana kuishi kwa amani na hivyo kichangia uthabiti na haki katika eneo hilo.

Kundi la Hamas linasemekana kuridhia mpango huo wa Marekani lakini Israel inajikokota ikisisitiza kwamba ni lazima iliangamize kabisa kundi la Hamas kabla ya kusitisha vita.

Imebainika pia kwamba Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anashinikizwa na watu fulani kwenye serikali yake kushikilia msimamo huo mkali.

Website | + posts