Home Habari Kuu Ruto ahakikishia Wakenya mabadiliko katika sekta ya kilimo

Ruto ahakikishia Wakenya mabadiliko katika sekta ya kilimo

0

Rais William Ruto amehakikishia Wakenya kwamba utawala wake umejitolea kuhakikisha mabadiliko katika sekta ya kilimo ili kupanua fursa kwa vijana na kutoa nafasi za ajira.

Akizungumza jana Jumapili wakati wa ibada ya madhehebu mbalimbali katika uwanja wa Amutala huko Kimilili katika kaunti ya Bungoma, kiongozi wa nchi alisema serikali imejitolea kusaidia wakulima kuongeza mazao.

Alihimiza wakulima kutumia fursa ya ruzuku ya serikali kwa mbolea kuongeza mazao.

Rais wakati huo huo aliahidi wakazi wa Bungoma kwamba serikali itakamilisha mpango wa kuunganisha umeme wa “last-mile electricity connectivity” ili kuhakikisha wengi wao wanapata huduma za umeme.

Ruto ambaye tayari ameondoka nchini kwa ziara rasmi nchini Korea Kusini, aliahidi ujenzi wa uwanja wa michezo wa kisasa pamoja na uwanja wa ndege wa kisasa katika kaunti ya Bungoma.

Awali, wakati wa sherehe za Madaraka, Rais alitangaza kufutiliwa mbali kwa madeni ya viwanda vya sukari vya eneo la magharibi mwa nchi ambayo yalikuwa zaidi ya shilingi bilioni 100.