Home Habari Kuu Rais Ruto afanya ziara rasmi nchini Japani

Rais Ruto afanya ziara rasmi nchini Japani

Ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha uhusiano wa kirafiki ulioko baina ya Kenya na Japan.

0

Rais William Ruto aliondoka nchini Jumatatu usiku kwenda nchini Japani kwa ziara rasmi ya kiserikali.

Kulingana na taarifa kutoka kwa msemaji wa Rais Hussein Mohamed, ziara hiyo inatarajiwa kuimarisha uhusiano wa kirafiki ulioko baina ya Kenya na Japani.

Ziara hiyo ya rais Ruto inajiri baada ya ziara rasmi iliyofanywa na waziri mkuu wa Japani Fumio Kishida humu nchini mwezi Mei mwaka jana na inaadhimisha miaka 60 ya uhusiano wa kibalozi baina ya mataifa haya mawili.

Wakati wa ziara hiyo, kiongozi wa taifa atafanya mazungumuzo na waziri mkuu wa taifa hilo Fumio Kishida, yatakayoangazia ushirikiano wa kiuchumi katika sekta muhimu za afya, teknolojia ya habari na nishati.

Kulingana na ikulu ya Nairobi, makubaliano kadha yanatarajiwa kutiwa saini ikiwemo ushirikiano wa kijeshi, ujenzi wa barabara na upanuzi wa maabara za taasisi ya utafiti wa matibabu nchini, KEMRI.

Makubaliano hayo yametajwa kuwa nguzo ya ushirikiano mpya baina ya mataifa haya mawili.

Website | + posts