Home Habari Kuu Rais Ruto awasili India kwa ziara ya siku mbili

Rais Ruto awasili India kwa ziara ya siku mbili

0

Rais William Ruto amewsili nchini India kwa ziara ya siku mbili leo Jumatatu baada ya kuhudhuria kongamano la tabia nchi la Umoja wa Mataifa, UN jijini Dubai katika Ufalme wa Milki za Kiarabu, UAE. 

Akiwa nchini India, Ruto atafanya mazungumzo na Waziri Mkuu Narendra Modi yatakayoangazia nyanja muhimu kama vile kilimo, biashara na uhamasishaji wa uwekezaji.

Aidha ukuzaji wa ushirikiano katika nyanja ya afya hasa uzalishaji wa dawa sawia na ushirikiano katika njanja za elimu, Habari, Mawasiliano na Teknolojia, ICT, masuala ya majini na nishati mbadala pia ni mambo yatakayojadiliwa.

Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu ya Nairobi Hussein Mohamed, kilele cha mazungumzo hayo kitakuwa kusainiwa kwa mikataba kadhaa ya maelewano inayokusudia kuimarisha uhusiano kati ya Kenya na India.

“Ziara hiyo ya kitaifa ni hatua kubwa katika uhusiano kati ya Kenya na India, ikitoa jukwaa kwa mipango ya ushirikiano na kuchangia manufaa ya pande mbili kati ya mataifa haya na watu wake,” alisema Mohamed katika taarifa leo Jumatatu.

Wakati wa ziara hiyo, Ruto pia atakutana na Rais Droupadi Murmu na kuhutubia kongamano la kibiashara na uwekezaji litakaloangazia ushirikiano mkubwa wa kiuchumi  kati ya Kenya na India.

 

 

Website | + posts