Home Habari Kuu Rais Ruto aahidi kutekeleza mpango wa maendeleo nchini

Rais Ruto aahidi kutekeleza mpango wa maendeleo nchini

0

Rais William Ruto amekamilisha ziara yake ya maendeleo ya siku tano katika eneo la Mlima Kenya.

Rais alizindua miradi ya maendeleo na kuwahutubia wakazi wa kaunti za Kiambu, Nyeri na Kirinyaga.

Amesema serikali itatimiza ahadi zake kwa Wakenya kupitia ajenda ya kutekeleza mabadiliko ya kiuchumi kutokea Chini kwenda Juu.

“Naenda kuongoza timu ambayo inaenda kuleta mabadiliko katika nchi yetu,” alisema kiongozi wa nchi.

Aliwahakikishia Wakenya dhamira ya serikali yake kupunguza gharama ya maisha kwa kuwaunga mkono wakulima kuongeza uzalishaji.

Leo Jumatano, Rais Ruto alizindua hospitali ya Naromoru Level 4 katika kaunti ya Nyeri.

Kadhalika alizindua miradi ya nyumba za bei nafuu katika maeneo ya Gichugu na Thika kando na kuzindua ujenzi wa bwawa la usambazaji maji katika kaunti ya Kiambu.

Naibu Rais Rigathi Gachagua, Magavana Mutahi Kahiga (Nyeri), Anne Waiguru (Kirinyaga), Kimani Wamatangi (Kiambu) na Waziri wa Afya Susan Nakhumicha ni miongoni mwa waliokuwapo wakati wa uzinduzi huo.

Rais alielezea kuwa serikali imepigia msasa utendakazi wa shirika la usambazaji wa vifaa tiba nchini, KEMSA kuhakikisha shirika hilo linanunua vifaa tiba kwa njia mwafaka na kwa uwazi.

Aliongeza kuwa serikali inawekeza katika kilimo, nyumba, utengenezaji bidhaa na uchumi wa dijitali ili kuongeza fursa kwa vijana.

“Tutabuni nafasi za ajira 500,000 kwa njia ya mtandao ili kuwaruhusu vijana wetu kuzifanyia kazi kampuni za kigeni wakiwa humu nchini ,” aliongeza Rais Ruto.

Akiwa mjini Thika alikofanya mkutano wa hadhara, aliwahakikishia wakazi na wafanyabiashara kwamba Kenya imechukua mwelekeo mzuri.

Kwa upande wake, Naibu Rais Rigathi Gachagua alitoa wito kwa viongozi kufanya kazi pamoja kwa manufaa ya raia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here