Rais William Ruto ameahidi kuungana na kushirikiana na viongozi wote waliochaguliwa katika kaunti ya Kisii wanapopanga maendeleo ya eneo hilo.
Akizungumza wakati wa hafla ya ibada iliyoandaliwa katika uwanja wa michezo wa Nyanturago, eneo bunge la Nyaribari Chache, huko Kisii, Rais alisema atashirikiana na viongozi wote katika maendeleo pasipo kuzingatia pande wanazoegemea kisiasa.
Alisema wananchi walitekeleza jukumu lao kwenye uchaguzi mkuu uliopita kwa kuwachagua na sasa ni wakati wa viongozi kuwafanyia wakenya kazi.
Kuhusu mradi uliokwama wa ujenzi wa tawi la Ibeno la taasisi ya kutoa mafunzo ya kimatibabu KMTC, Rais alisema ataukamilisha.
Alishukuru wapiga kura wa eneo la Nyaribari Chache kwa kuchagua mbunge wa chama cha UDA Zaheer Jhanda ambaye anasema ni mchapa kazi akiahidi kumwelekeza ifaavyo kwani yeye ni mwalimu wa siasa.
Rais alikubali kushirikiana na Gavana Simba Arati kujenga uwanja wa michezo wa Nyanturago ambapo atatuma waziri wa michezo ashauriane na Simba ili kuweka mikakati ya ujenzi wa uwanja huo.
Ardhi iliyotengewa uwanja wa ndege huko Suneka alisema itaelekezwa kwa matumizi tofauti yenye manufaa kwa wakazi wa Kisii kwa sababu utafiti ulionyesha kwamba eneo hilo halifai kuwa uwanja wa ndege. Aliahidi kufanikisha ujenzi wa uwanja wa ndege huko Nyangusu iwapo makubaliano yataafikiwa kati ya viongozi wa Kisii.