Aliyekuwa Rais wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi, ameaga dunia, akiwa na umri wa miaka 99.
Akitangaza kifo hicho, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, alisema Rais huyo mstaafu alifariki katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam siku ya Alhamisi.
” Ndugu wananchi, kwa majonzi makubwa nasikitika kutangaza kifo cha Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, ambaye amefariki dunia leo Alhamisi tarehe 29 Februari mwaka 2024 saa 11:30 jioni, katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena, Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa Saratani ya Mapafu,” alisema Rais Samia.
Rais huyo mstaafu Hassan Mwinyi alikuwa akiugua ugonjwa wa saratani ya mapafu.
Rais Samia amesema taifa hilo litaomboleza kwa siku saba.
“Nchi yetu itakuwa katika kipindi cha siku saba za maombolezo, ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia kesho Machi 1, 2024,” aliongeza Rais Samia .
Kulingana na Rais Samia, hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi atazikwa tarehe 2 Machi 2024 Unguja, kisiwani Zanzibar.
Ali Hassan Mwinyi aliongoza Serikali ya awamu ya Pili, aliingia madarakani rasmi tarehe 5 Novemba 1985.