Home Kimataifa Rais Lula abadili msimamo kuhusu usalama wa Putin nchini Brazil

Rais Lula abadili msimamo kuhusu usalama wa Putin nchini Brazil

0

Kiongozi wa nchi ya Brazil Rais Luiz Inacio Lula da Silva amebadilisha msimamo wake kuhusiana na usalama wa Rais wa Urusi Vladmir Putin nchini Brazil wakati wa kongamano la G20 mwaka ujao.

Awali Rais Lula ambaye alizungumza pembezoni mwa kongamano la G20 nchini India alisema kwamba Putin hatakamatwa iwapo atahudhuria kongamano la mwaka ujao la G20 nchini Brazil.

Sasa Lula anasema uamuzi wa kumkamata au kutomkamata Putin nchini Brazil kulingana na kibali kilichotolewa na mahakam ya kimataifa ya jinai ICC ni wa idara ya mahakama nchini humo.

Inahitajika kwamba nchi zote ambazo zilitia saini sheria ya Roma ambayo ilibuni mahakama ya ICC zisaidie mahakama hiyo kumtia mbaroni yeyote ambaye mahakama ya ICC imetoa kibali cha kumkamata.

Rais Lula da Silva anaonekana kughadhabishwa na sheria hiyo ya Roma akisema kwamba nchi zinazostawi hutia saini makubaliano na sheria ambazo huishia kuziathiri vibaya.

“Nataka kujua ni kwa nini sisi ni washiriki wa sheria iliyobuni mahakama ya ICC na wala sio Marekani au China? aliuliza Rais Lula akifafanua kwamba hatajiondoa kwa mahaka ahiyo ya kimataifa lakini antaka kujua ni kwa nini Brazil ni mshirika.

Putin alikosa kuhudhuria kongamano la mwaka huu la kundi la mataifa 20 yaliyostawi ulimwenguni almaarufu G20 kuzuia mzozo wa kisiasa na hata uwezekano wa kutiwa mbaroni.

Mwezi machi mahakama ya ICC ilitangaza utoaji wa kibali cha kukamatwa dhidi ya Vladmir Putin Rais wa Urusi kwa makosa ya kivita.

Urusi nayo ilijibu kwa kutoa kibali cha kukamatwa dhidi ya kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya ICC Karim Khan, mwezi Mei.

Brazil ni mojawapo ya nchi ambazo zilitia saini sheria ya Roma iliyobuni mahakama ya ICC. Sheria hiyo iliratibishwa huko Roma Julai 17, 1998 na kuanza kutekelezwa Julai 1, 2002.