Rais wa Marekani Joe Biden, ameshiriki meza ya mazungumzo na maafisa wa usalama, huku taharuki ikizidi kuongezeka kuhusu Iran kuishambulia Israel.
Iran inalenga kulipiza kisasi baada ya kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh kuuawa nchini humo, huku ikiilaumu Israel kwa kutekeleza shambulizi hilo.
Hadi kufikia sasa, Israel haijasema lolote kuhusu kuhusika kwake katika mauaji hayo.
Katika mkutano huo, Biden alifahamishwa kuhusu mipango ya kuunga mkono Israel iwapo itashambuliwa.
Mataifa kadhaa yamewatahadharisha raia wao dhidi ya kusafiri Israel, huku walio Lebanon wakiagizwa kuondoka.
Hata hivyo haijabainika ni wakati upi mashambulizi hayo yataanza, lakini awali Blinken alidokeza kuwa huenda yakatekelezwa ndani ya saa 24 au 48 kuanzia jana Jumatatu.