Home Habari Kuu Rais azindua vifaa vya wahudumu wa afya kwa jamii

Rais azindua vifaa vya wahudumu wa afya kwa jamii

0

Rais William Ruto amesema kwamba katika muda wa siku chache zijazo, Wakenya hawatahitajika kusafiri hadi vituo vya afya kufanyiwa vipimo vya kila mara na kutibiwa magonjwa madogo madogo.

Akizungumza katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi wakati wa kuzindua msafara wa kusambaza vifaa 100,000 vya matibabu vitakavyotumiwa na wahudumu wa afya kwa jamii nyanjani, Rais alisema wahudumu hao watasaidia kufikishia Wakenya huduma nyumbani.

Kulingana naye, mpango huo ni ishara ya kujitolea kwa serikali kuimarisha maisha ya Wakenya wa tabaka la chini kwanza chini ya mpango wa serikali uitwao, “Bottom-up transformation of citizen services”.

Rais aliahidi kwamba wahudumu hao watapokea marupurupu yao ya kila mwezi kwa wakati unaofaa, kuanzia mwezi ujao.

Alisema serikali ya kitaifa imekubaliana na serikali za kaunti kuhusu namna ya kutoa malipo kwa wahudumu hao.

Kila mhudumu wa afya wa jamii aliyehudhuria hafla hiyo alipokea mkoba ambao una vifaa ambavyo vitamsaidia kutekeleza majukumu yake nyanjani.

Naibu Rais Rigathi Gachagua kwa upande wake alipongeza Rais kwa kuzindua mpango huo baada ya mwaka mmoja tu mamlakani akisema kwamba wahudumu hao wa afya nyanjani watatoa huduma za msingi kwa wakenya vijijini na katika kaunti ambazo zitasaidia kutambua magonjwa mapema, kutoa huduma za kuzuia magonjwa pamoja na za kuboresha afya.

Waziri wa afya Susan Nakhumicha alisema mkakati wao ni kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma akisema wahudumu wa afya ya jamii waliozinduliwa leo pamoja na vifaa vyao watasaidia kuafikia lengo lao.

Alisema hii ni hatua nzuri katika kuafikia mpango mkuu wa afya bora kwa wote.