Home Kimataifa Rais apokea ripoti ya kikosi kazi kuhusu mabadiliko katika idara ya polisi

Rais apokea ripoti ya kikosi kazi kuhusu mabadiliko katika idara ya polisi

0
kra

Rais William Ruto leo amepokea ripoti kutoka kwa kikosi kazi kuhudu mabadiliko katika idara ya polisi nchini kilichokuwa chini ya uenyekiti wa aliyekuwa jaji mkuu David Maraga.

Rais amekubali mapendekezo matatu ya kikosi kazi hicho.

kra

Pendekezo la kwanza ni kuhamisha huduma ya taifa ya polisi, huduma ya magereza na huduma ya vijana kwa taifa hadi sekta ya ulinzi kwa kuzingatia malipo yao na masharti ya kazi.

Rais alisema kwa kutekeleza hilo, maafisa katika huduma hizo tatu watapokea mishahara na masharti mengine ya kazi yanayoambatana na kazi ambayo wanafanya.

La pili ni viwango viwili vya kujiunga na huduma ya taifa ya polisi cha kwanza kikiwa kuingia kama makonstebo na kiwango cha pili kikiwa cha makadeti.

Tume ya huduma ya taifa ya polisi itaamua vigezo vya kuhitimu kujiunga kupitia viwango hivyo viwili.

“Wakati huu ambapo uhalifu unazidi kubadilika, pendekezo hili litavutia wataalamu zaidi kwa huduma ya taifa ya polisi.” Alisema Rais Ruto.

Pendekezo la tatu la kikosi cha Maraga ni utekelezaji wa sera ya uhamisho wa maafisa wa huduma ya taifa ya polisi kwamba hakuna afisa atakayeruhusiwa kusalia kwenye kituo kimoja kwa zaidi ya miaka mitatu.

Rais alikubali pendekezo hilo akiongeza kusema kwamba katika siku zijazo hakuna afisa wa polisi ambaye atapandishwa cheo ilhali amehudumu kwenye kituo kimoja tu.

Maraga alisema ripoti ya mwisho ya kikosi kazi hicho kuhusu mabadiliko katika idara ya polisi itatolewa katika muda wa mwezi mmoja ujao.

“Ninahakikishia maafisa wa polisi kujitolea kwetu kuimarisha huduma ya polisi, ikiwemo mishahara yao na masharti mengine ya kazi.” alisema Rais William Ruto wakati wa kupokea ripoti hiyo.

Wengine waliokuwepo wakati wa kutolewa kwa ripoti hiyo ya mabadiliko yanayohitajika katika huduma ya taifa ya polisi ni Naibu Rais Rigathi Gachagua, waziri aliye na mamlaka makuu Musalia Mudavadi, Mawaziri Kithure Kindiki wa mambo ya ndani na Aden Duale wa ulinzi pamoja na mwanasheria mkuu JB Muturi.

Wengine ni Inspekta Jenerali wa polisi Japheth Koome, manaibu inspekta jeneraki Douglas Kanja na Noor Gabow, mwenyekiti wa tume ya huduma ya taifa ya polisi Eliud Kinuthia na wanachama wa kikosi kazi cha mabadiliko katika idara ya polisi.

Website | + posts