Home Habari Kuu Raila: Sijamuidhinisha Kalonzo kuwania urais 2027

Raila: Sijamuidhinisha Kalonzo kuwania urais 2027

0
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka akiwa na kinara wa Azimio Raila Odinga
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka akiwa na kinara wa Azimio Raila Odinga

Kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga amekanusha madai kuwa amemuidhinisha kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka kuwa mgombea urais wa muungano huo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. 

Kulikuwa na dhana kuwa Raila amemuidhinisha Kalonzo kutifua kivumbi dhidi ya Rais William Ruto wakati wa uchaguzi huo baada ya kiongozi huyo wa chama cha ODM kummiminia sifa tele Kalonzo.

Raila anasema bado imesalia miaka minne kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu na ni mapema mno kwa chama chochote cha kisiasa kumuidhinisha yeyote kuwa mgombea wake wa urais.

Haijabainika ikiwa Raila atawania urais wakati wa uchaguzi huo na kunao wanaokisia kuwa baada ya kujaribu kushika hatamu za uongozi wa nchi mara tano bila mafanikio, huenda akamuunga mkono Kalonzo kujaribu bahati yake.

“Bw. Odinga anabainisha kuwa sifa zake kwa Kalonzo kwa kusimama naye katika chaguzi tatu zilizopita mtawalia, maadili mema ya Kikristo ya kiongozi huyo wa chama cha Wiper na uungwaji mkono ambao Kalonzo amejizolea kote nchini haimaanishi kuwa Raila amemuidhinisha Kalonzo kuwa mgombea urais wa Azimio mwaka 2027,” alisema Raila kupitia kwa msemaji wake Dennis Onyango.

“Bw. Odinga anaiona Azimio kama muungano wenye washindani sawa, ambapo kila kiongozi ana fursa sawa ya kuwa mgombea wa urais mnamo mwaka 2027, kulingana na uhusiano wa kila kiongozi na wanachama wa muungano huo. Hata hivyo, mgombea huyo hatatajwa hadi isalie tu miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.”

Hata hivyo, Raila anaamini kuwa ikiwa uchaguzi huru na wa haki utaandaliwa, Kalonzo ana makali ya kumbwaga Rais Ruto debeni, kinyume cha kauli za Rais Ruto kuwa itakuwa rahisi zaidi kumtema Kalonzo kwenye kinyang’anyiro cha urais.