Home Taifa Raila: ODM wala Azimio haijajiunga na serikali ya Rais Ruto

Raila: ODM wala Azimio haijajiunga na serikali ya Rais Ruto

0
kra

Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga amekanusha madai kwamba chama hicho kimeunda serikali ya muungano na chama tawala cha UDA. 

Raila ambaye ameshutumiwa vikali kwa kusaliti ari ya mabadiliko inayoshinikizwa na vijana wa Gen Z, aidha amekanusha madai kuwa muungano wa Azimio umejiunga na serikali ya Kenya Kwanza.

kra

Kulingana na Raila, walitazamia masharti ya uteuzi wa wanachama wake kuwekwa wazi kabla ya kufanyika kwake.

“Tulikuwa tumetarajia kuratibiwa kwa masharti bayana ya ushirikiano kwa kuzingatia masuala mbalimbali tuliyoibua katika taarifa yetu ya awali,” alisema Raila katika taarifa.

Ilikuwa ni mara ya kwanza alizungumzia uteuzi huo tangu hiyo jana.

“Ingawa tunawatakia kila la heri walioteuliwa na kuamini kuwa watachangia kwa njia chanya maendeleo ya taifa, tunaendelea kuunga mkono kufanyika kwa mazungumzo ya kitaifa chini ya masharti tuliyoelezea awali.”

Masharti hayo ni pamoja na kufidiwa kwa familia zilizopoteza jamaa wao wakati wa maandamano na kuachiliwa huru kwa wale wote waliokamatwa.

Matamshi ya Raila yanakuja wakati anakabiliwa na shutuma ya kuwa kibaraka na kuwasiliti vijana wa Gen Z ambao wamekuwa wakiandamana kushinikiza utawala bora nchini.

Kiasi kwamba baadhi ya wabunge wa ODM wamejitenga na uteuzi huo.

Wanachama wa ODM walioteuliwa na Rais William Ruto kujiunga na Baraza Jipya la Mawaziri ni pamoja na waliokuwa Magavana Hassan Joho (Wizara ya Madini), Wycliffe Oparanya (Waziri wa Vyama vya Ushirika), John Mbadi (Waziri wa Fedha) na Opiyo Wandayi (Waziri wa Nishati).