Home Habari Kuu Raila kutoa msimamo kuhusu ripoti ya maridhiano Alhamisi

Raila kutoa msimamo kuhusu ripoti ya maridhiano Alhamisi

0
Kiongozi wa muungano wa upinzani wa Azimio Raila Odinga atatoa mwelekeo kuhusu ripoti ya kamati ya kitaifa ya maridhiano Alhamisi wiki hii.
Hii ni baada ya kukutana na uongozi wa muungano huo ikiwa ni pamoja na wabunge.
Raila anasema ripoti hiyo itachambuliwa kwa mapana na marefu na wanachama wa Azimio kupewa fursa ya kuijadili kabla ya azimio kufikiwa.
Akizungumza mjini Nyamira leo Jumatatu, Raila alisema Wakenya wana shauku ya kubaini kilichomo katika ripoti hiyo na msimamo wa Azimio kuihusu, hivyo haja ya kuichambua vilivyo.
Alitoa wito kwa wafuasi wa muungano huo na Wakenya kwa jumla kumpa hadi siku ya Alhamisi ili kufahamu msimamo wake kuhusu ripoti hiyo, idara ya mawasiliamo ya chama cha ODM imesema katika taarifa.
Ripoti hiyo imekuwa chanzo cha migawanyiko katika muungano wa Azimio huku kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa akiapa kutoiunga mkono kwa misingi kwamba haikuangazia suala kuu linalowaathiri Wakenya ambalo ni gharama ya juu ya maisha.
Maoni sawia yametolewa na kiongozi wa chama cha Narc K Martha Karua.
Kamati ya kitaifa ya maridhiano ilisimamiwa na kiongozi wa wengi katika bunge la Taifa Kimani Ichung’wah na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ambaye ni mwanachama wa Azimio.