Home Kimataifa Raila awataka Mawaziri Chirchir na Ndung’u kujiuzulu

Raila awataka Mawaziri Chirchir na Ndung’u kujiuzulu

0
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga.
kra

Kiongozi wa muungano wa Azimio Raila Odinga sasa anawataka Mawaziri Davis Chirchir wa Nishati na Prof. Njuguna Ndung’u wa Fedha kujiuzulu na kushtakiwa. 

Kiini cha wito wake ni utata unaozingira umiliki na uagizaji wa shehena ya mafuta yenye thamani ya shilingi bilioni 17.

kra

Mfanyabiashara Anne Njeri alidai kuagiza mafuta hayo, madai ambayo serikali imeyapuuzilia mbali vikali.

Waziri Chirchir anasema stakabadhi ambazo Njeri anadai kutumia kuagiza mafuta hayo ni ghushi.

Huku akidai Njeri alitumiwa tu na watu mashuhuri walionuia kubadhiri rasilimali za umma, Raila anawanyoshea kidole cha lawama Mawaziri Chirchir na Prof. Ndung’u kutokana na matumizi ya shilingi bilioni 17 zilizotumiwa kuagiza mafuta hayo akisema walikiuka katiba.

“Bw. Chirchir na Waziri wa Fedha Njuguna Ndung’u bila shaka wametekeleza makosa ya jinai, kutumia vinaya ofisi na kukiuka katiba. Waliiba fedha za umma mbali na kutumia fedha kuliko kiwango kilichoidhinishwa na serikali. Sio tu kwamba wanapaswa kujiuzulu bali pia wanapaswa kushtakiwa,” alisema Raila wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumatatu.

Siku chache zilizopita, Raila alidai kuwa Kenya haijatia saini mkataba wowote na Saudi Arabia, bali mkataba kati ya nchi hizo ulikuwa ni kati ya Wizara ya Nishati ya Kenya na kampuni za mafuta zinazomilikiwa na serikali ya Saudia.

Raila kadhalika alidai mkataba huo unachangia kupanda kwa bei ya mafuta nchini na kuwafaidi baadhi ya maafisa wa serikali ya Kenya Kwanza, madai ambayo yamekemewa na kiongozi wa wengi katika bunge la taifa Kimani Ichung’wah

Kupitia taarifa aliyopachika katika mtandao wake wa X, Ichung’wa alitaja madai ya Raila kuwa propaganda za kisiasa na njama za kufufua umaarufu wake wa kisiasa ambao umedidimia.

“Madai ya Raila Odinga  ni propaganda za kisiasa na uvumi. Madai hayo hayana msingi wala ushahidi,” alisema  Ichung’wah.

Rais William Ruto ameutetea mkataba huo akisema ulifanywa kwa njia sahihi na ulijawa na wingi wa ubunifu.

Website | + posts