Home Habari Kuu Raila apendekeza majadiliano kuhusu mradi wa nyumba

Raila apendekeza majadiliano kuhusu mradi wa nyumba

0

Raila Odinga kiongozi wa muungano wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya anapendekeza kikao na serikali na wadau kujadili utekelezaji wa mradi wa nyumba za bei nafuu.

Odinga anataka Rais William Ruto awezeshe kuandaliwa kwa mdahalo wa kitaifa kuhusu mradi huo kwa kutoa jukwaa ambalo wakenya wanaweza kutumia kutoa maoni yao.

Kulingana naye ni muhimu kila mkenya afahamu jinsi mradi huo unaendeshwa na katika ufahamu huo basi watakuwa na imani nao.

Kiongozi huyo alitoa mfano wa mambo yalivyokuwa wakati wa utawala wa Rais Mwai Kibaki akisema miradi mingi ilifanikiwa wakati huo kwa sababu walikuwa wanajadiliana kila mara na wataalamu na wadau wengine.

Anaelezea kwamba wakati huo kuliandaliwa mkutano uliopatiwa jina la “Kenya tunataka” au “Kenya We Want” ambapo watu walijadili na kukubaliana kuhusu kilichohitajika kutekelezwa.

Raila aligusia pia kubuniwa kwa baraza la kitaifa la masuala ya kijamii na kiuchumi ambalo wanachama walikuwa wataalamu wa humu nchini na wa nje.

“Na hivyo ndivyo tuliafikia mpango wa maendeleo wa Vision 2030, reli ya kisasa SGR na miradi mingine.” alisema Raila.

Hisia zake ni kwamba serikali ya sasa ilishauriwa visivyo kuendesha mradi huo kwa njia ambayo imesababisha wakenya wengi kupinga ushuru wa nyumba za bei nafuu.

Kwa maoni yake sio jambo la busara kumfanya kila mmoja alipie ujenzi wa nyumba hizo ilhali hajahakikishiwa kwamba atanufaika.

Alikuwa akizungumza alipoongoza maadhimisho ya miaka 15 ya chama cha PNU.

Website | + posts