Home Taifa Raila amwomboleza Makamu wa Rais wa Malawi

Raila amwomboleza Makamu wa Rais wa Malawi

0

Kinara wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga ametuma risala za rambirambi kwa taifa la Malawi kufuatia kifo cha Makamu wa Rais Dkt. Saulos Klaus Chilima na wengine tisa walioangamia katika ajali ya ndege.

“Tunaungana na wananchi wa Malawi na Afrika nzima kuomboleza kifo cha Makamu wa Rais wa Malawi Dkt. Saulos Klaus Chilima na wenzake tisa katika ajali ya ndege jana. Pole sana Rais Lazarus Chakwera na wananchi wa Malawi kwa msiba huu mzito,” alisema Raila kupitia mtandao wa X.

Chilima alifariki siku ya Jumatatu pamoja na wengine tisa kwenye ndege ya kijeshi ya Malawi.

Jeshi la Malawi lilisema ndege hiyo ‘ilipotea kwenye rada’ baada ya kuondoka mjini Lilongwe Jumatatu asubuhi.

“Juhudi zote za mamlaka ya usafiri wa anga kuwasiliana na ndege hiyo tangu iliporuka rada zimeshindwa hadi sasa,” Katibu wa Ofisi ya Rais na Baraza la Mawaziri, Colleen Zamba alisema.

Zamba alisema ndege hiyo, iliyoondoka katika mji mkuu Lilongwe saa tatu na dakika 17 asubuhi (saa za Malawi), ilishindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzuzu saa nne na dakika mbili asubuhi Jumatatu kama ilivyopangwa, na kwamba juhudi za mamlaka ya anga kuwasiliana na nayo zilishindikana.

Kifo cha Chilima kilitangazwa rasmi na Rais Chakwera siku ya Jumanne akisema ndege hiyo ilianguka kwenye mlima na hakuna aliyenusurika.

Chilima mwenye umri wa miaka 51, alichukua hatamu ya makamu wa rais kwa mara ya kwanza Mei 30, 2014. Aliapishwa tena kwa wadhifa huo Juni 28, 2020. Alikuwa na mke mmoja na watoto wawili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here