Raila Odinga kiongozi wa muungano wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya amekosoa maafisa wa polisi kwa kile alichokitaja kuwa matumizi ya nguvu kupita kiasi wakati wa maandamano.
Odinga ambaye pia ni kiongozi wa chama cha ODM alisema maafisa hao wa polisi walitumia nguvu dhidi ya wakenya waliokuwa wakiandamana kwa njia ya amani na wanahabari tarehe 8 mwezi huu.
Alisema katiba inakubalia maandamano ya amani na hivyo polisi hawafai kuwakamata na kuwazuilia waandamanaji au kutumia nguvu kupita kiasi dhidhi yao.
Waziri huyo mkuu wa zamani alisema vitendo vya polisi siku ya Alhamisi havikubaliki kwa sababu ni ukiukaji wa haki kuambatana na katiba.
Raila alisema kuwa maafisa ni sharti waheshimu haki za kikatiba za wakenya wote. Alitoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa wakenya wote wanaozuiliwa bila sababu.
Kulingana naye, mienendo ya maafisa wa polisi walionyanyasa wakenya wasio na hatia inafaa kuchunguzwa na wahusika wachukuliwe hatua za kisheria.
Taarifa ya Odinga inajiri baada ya maafisa wa polisi kutumia kila mbinu kutawanya wakenya waliokuwa wakiandamana jijini Nairobi tarehe 8 mwezi wa 8 mwaka 2024.
Waliokusanyika jijini walirushiwa vitoza machozi na polisi huku wengine wakikamatwa. Maandamano yamekuwa ya kiendelea kwa muda nchini kushinikiza utawala bora.