Home Habari Kuu Raila afanya mkutano na mabalozi wa Misri na Uholanzi

Raila afanya mkutano na mabalozi wa Misri na Uholanzi

0

Kinara wa ODM Raila Odinga leo Jumatano amefanya mkutano na mabalozi wa Misri Wael Nasreldin Attiya na Uholanzi Maarten Brouwer.

Kwenye mkutano uliofanyika nyumbani kwake huko Karen jijini Nairobi, Raila alisema walizungumzia uwezekano wa kuwa na Afrika yenye nguvu na umoja ambapo alisisitiza haja ya ushirikiano wa bara, kuimarishwa kwa biashara na maendeleo ya miundombinu.

Katika mazungumzo na mabalozi hao, Raila alielezea wasiwasi wake kuhusu ukabila na mawazo endelevu ya “wao dhidi yetu” katika uongozi na ugawaji wa rasilimali.

Alisisitiza haja ya kuwa na mpango wa hatua kwa hatua wa kushughulikia changamoto kama vile sarafu tofauti, mahitaji ya visa na sheria zisizolingana za trafiki ya anga.

“Nilisisitiza umuhimu wa mbinu ya hatua kwa hatua ya mageuzi ya kushughulikia masuala kama vile sarafu nyingi, mahitaji mengi ya viza, na kanuni mbalimbali za udhibiti wa usafiri wa anga. Ninaamini wakati umefika wa kuanzishwa kwa pasipoti ya AU ili kurahisisha usafiri kote Afrika,” alisema Raila.

Raila pia alizungumzia changamoto kama vile njia za malipo ya bidhaa zinazouzwa kati ya mataifa ya Afrika huku kukiwa na uhaba wa dola za Marekani na umuhimu wa kuwezesha uhuru wa kutembea kwa watu wao.

Kiongozi huyo wa Azimio alitumia fursa hiyo kueleza maono yake kwa Afrika katika mazingira yanayoendelea duniani na jitihada zake za kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC)

Mkutano huo pia ulizungumzia haja ya kutekelezwa kwa mikataba ya biashara zaidi ya kutia saini tu.

Mkwewe Ida Odinga alikuwepo kwenye mkutano huo.