Aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga anaendelea kusisitiza kwamba chama chake cha Orange Democratic Movement – ODM hakijaingia kwenye muungano tawala wa Kenya Kwanza na hakuna makubaliano kati ya chama hicho na serikali.
Raila anasema kwamba chama cha ODM bado kipo kwenye muungano wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya akielezea kwamba hana shida kuona wanachama wa chama chake wakiteuliwa kuhudumu kwenye serikali ya Rais Ruto.
Waziri huyo mkuu wa zamani anawataka wanachama wa ODM walioteuliwa kuwa mawaziri waendeleze sera za chama hicho hata wanapotekeleza majukumu yao mapya iwapo wataidhinishwa.
Mwaniaji huyo wa wadhifa wa mwenyekiti wa tume ya umoja wa Afrika aliyasema hayo katika kijiji cha Nyachwinya karibu na mji wa Siaya kwenye hafla ya mazishi ya Evans Umidha Orwenjo.
Wakati huo huo Raila alisema kwamba maswala yaliyoibuliwa na wakenya wa umri mdogo almaarufu Gen Z ambao wamekuwa wakiandamana dhidi ya serikali sio mapya, ni yale ambayo upinzani umekuwa ukupigania tangu zamani.
Alitoa mfano wa mwaka jana ambapo wafuasi wa upinzani waliandamana kulalamikia ufisadi, gharama ya juu ya maisha, ushuru wa kiwango cha juu na ukosefu wa maadili kati ya viongozi.
Katika orodha ya pili ya mawaziri wateule, Rais William Ruto aliwateua wanachama wanne wa chama cha ODM ambao ni John Mbadi ambaye amependekezwa kuwa waziri wa fedha, Hassan Joho ambaye amependekezwa kuwa waziri wa madini, Opiyo Wandayi waziri wa Kawi na Wycliff Oparanya waziri wa vyama vya ushirika.