Home Burudani Raia wa Tanzania waibuka washindi wa AGT: Fantasy League

Raia wa Tanzania waibuka washindi wa AGT: Fantasy League

0
Ramadhani Brothers na kocha wao Howie Mandel

Ibrahim Ramadhan na nduguye Fadhili Ramadhan ambao wanafahamika kama Ramadhan Brothers ndio washindi wa awamu ya kwanza Fantasy League ya mashindano ya talanta almaarufu America’s Got Talent – AGT.

Wawili hao ambao sanaa yao ni maonyesho ya sarakasi walijinyakulia zawadi kuu ambayo ni dola elfu 250 za kimarekani, sawa na milioni 637.5 za Tanzania.

America’s Got Talent ni mashindano ambayo yalianzia nchini Marekani mwaka 2006 na baadaye kuelekezwa katika maeneo mengine ulimwenguni.

America’s Got Talent Fantasy League ni tofauti kidogo ambapo majaji wanachagua washindani waliowapendelea kwenye mashindano ya awali na kila jaji ana washindani anaowanoa makali na inakuwa kana kwamba wote wako kwenye mashindano.

Majaji Mel B, Simon Cowell, Heidi Klum na Howie Mandel walipatiwa washindani 40 wa awali katika AGT ambapo kila mmoja alichagua washindani 10 wa kufunza.

Shindano liliendelea kama kawaida ambapo mchujo ulifanyika na mwisho wakasalia washindani watano ambao walihusika kwenye onyesho la mwisho wa msimu, Jumatatu Februari 19, 2024.

Washindani hao ni mcheza densi Musa Motha, kwaya ya Sainted, kundi la densi na sarakasi la V. Unbeatable, kundi la kucheza ala za muziki Pack Drumline na kundi la sarakasi la Ramadhani Brothers.

Ramadhani Brothers walishiriki katika mashindano hayo kwa mara ya kwanza mwaka 2023 kwenye msimu wa 18 wa America’s Got Talent na wakawa nambari 5.

Walikuwa kwenye kundi la mkufunzi na jaji Howie Mandel.

Ndugu hao waliojawa na furaha baada ya kutangazwa washindi walisema kwamba kushinda kwenye Fantasy League ni hatua kubwa sana ikitizamiwa kwamba wameshinda hata washindi wa awali wa AGT.

Website | + posts