Home Habari Kuu Raia wa Marekani, Uhispania na Czech wazuiliwa nchini Venezuela

Raia wa Marekani, Uhispania na Czech wazuiliwa nchini Venezuela

0
Waziri Diosado Cabello
kra

Venezuela imewazuilia raia watatu wa Marekani, Wahispania wawili na raia wa Czech kutokana na madai ya njama ya kuyumbisha taifa hilo la Amerika Kusini. Haya ni kulingana na afisa mmoja mkuu serikalini.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Venezuela Diosdado Cabello alisema Jumamosi kwamba sita hao walikamatwa kwa tuhuma za kupanga shambulizi dhidi ya Rais Nicolas Maduro na serikali yake.

kra

Kukamatwa kwa watu hao kunajiri wakati mvutano unaongezeka katika wiki za hivi karibuni kati ya Venezuela na Marekani, Uhispania na mataifa mengine ya Magharibi kuhusu uchaguzi wa Venezuela unaozozaniwa, uliofanyika mwisho wa Julai.

Maduro ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2013 alitangazwa mshindi wa kura hiyo, lakini upinzani wa nchi hiyo umesema kinyang’anyiro hicho kilikumbwa na udanganyifu na kwamba mgombea wake amemshinda rais huyo wa muda mrefu.

Matokeo ya uchaguzi huo yalichochea maandamano makubwa ya upinzani na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 24 na karibu 200 kujeruhiwa.

Wakati wa mkutano na wanahabari Jumamosi, Cabello aliwashutumu raia hao wawili wa Uhispania waliozuiliwa kwa madai ya kuwa na uhusiano na huduma ya siri ya Uhispania na kupanga mauaji ya meya.

Wawili hao walikamatwa wakipiga picha katika mji wa Puerto Ayacucho kulingana na waziri huyo.Vyombo vya habari vya Uhispania viliripoti kuwa serikali ya Uhispania ilikanusha dai hili.

Cabello pia aliwashutumu raia watatu wa Marekani na raia wa Czech kwa kuhusika na vitendo vya kigaidi ikiwa ni pamoja na madai ya mipango ya kumuua Maduro na maafisa wengine.

“Makundi haya yanatafuta kunyakua utajiri wa nchi na sisi kama serikali tutajibu kwa uthabiti jaribio lolote” Cabello alisema.

Aliongeza kuwa takriban bunduki 400 kutoka Marekani zimekamatwa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba “mwanajeshi wa Marekani” alikuwa amezuiliwa nchini Venezuela na kwamba inafahamu ripoti ambazo hazijathibitishwa za raia wawili wa ziada wa Marekani kuzuiliwa huko.

Lakini Wizara ya Mambo ya Nje ilisema Marekani haikuhusika katika jaribio la kumwondoa Maduro madarakani.

“Madai yoyote ya kuhusika kwa Marekani katika njama ya kumpindua Maduro ni ya uwongo kabisa,” msemaji huyo alisema. “Marekani inaendelea kuunga mkono suluhu la kidemokrasia kwa mzozo wa kisiasa nchini Venezuela.”

Venezuela ilimwita balozi wake nchini Uhispania wiki hii kwa mashauriano na kumwita balozi wa Uhispania kufika katika Wizara ya Mambo ya Nje baada ya waziri wa Uhispania kumshutumu Maduro kwa kuendesha “dikteta”.

Venezuela pia ilikasirishwa na uamuzi wa Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez kukutana na mgombea wa upinzani wa Venezuela Edmundo Gonzalez, ambaye alienda uhamishoni nchini Uhispania wiki iliyopita baada ya kutishiwa kukamatwa na serikali ya Maduro’.

Caracas pia amekuwa na mvutano mpya na Washington, ambayo ilimtambua Gonzalez kama mshindi wa uchaguzi wa Julai 28.

Marekani pia iliiwekea Venezuela vikwazo vipya mapema wiki hii.

Website | + posts