Home Habari Kuu Raia wa kwanza wa kigeni watua nchini bila viza

Raia wa kwanza wa kigeni watua nchini bila viza

0

Kundi la kwanza la raia wa kigeni leo Ijumaa liliwasili nchini bila hitaji la viza.

Lilakiwa na Katibu katika Idara ya Uhamiaji Prof. Julius Bitok punde baada ya kuwasili katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta, JKIA.

Raia hao wa kigeni wanaotoka mataifa mbalimbali duniani ni sehemu ya zaidi ya wageni 500 ambao tayari wameidhinishwa chini ya mfumo wa usafiri wa kielektroniki.

Prof. Bitok anasema kufikia sasa, nchi hii imepokea maombi zaidi ya  3,200 kwenye mfumo huo.

Aliwahakikishia wageni wanaowasili nchini au wenye nia kama hiyo kwamba mfumo huo ni salama kwani habari kuhusu wageni hupokelewa na kukaguliwa kabla hawajawasili humu nchini.

Kulingana naye, mfumo huo umeimarishwa ili kurahisisha usafiri na hivyo kuwavutia wawekezaji na watalii zaidi humu nchini.

Wale wanaoidhinishwa kuingia nchini kupitia mfumo huo wanaruhusiwa kukaa humu nchini kwa kipindi cha siku 90.

Gharama ya mfumo huo ni shilingi 4,710 sawa na dola 30 za Marekani.

Tangazo kwamba raia wote wa nchi za kigeni kutoka kila pembe ya dunia wataingia nchini bila viza kuanzia mwezi Januari mwaka 2024 lilitolewa na Rais William Ruto.

“Kuanzia mwaka 2024, hautahitaji viza kuingia nchini Kenya. Haitahitajika kamwe kwa mtu yeyote kutoka sehemu yoyote ya dunia kubeba mzigo wa kutuma maombi ya viza ili kuja nchini Kenya,” alitangaza Rais Ruto wakati akiongoza taifa kuadhimisha sherehe za Jamhuri.

Hatua hiyo inaifanya Kenya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuwaondolea raia wote wa kigeni hitaji la viza.

Rwanda, Benin, Gambia na Ushelisheli zimetangaza kuondoa hitaji la viza lakini kwa Waafrika wanaoingia katika nchi hizo.

 

Website | + posts