Raia 8 wa kigeni wamekatwa na maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai mjini Kitale kaunti ya Trans Nzoia.
Washukiwa hao wanaojumuisha raia wa Somalia na Uganda, walitiwa nguvuni kama sehemu ya msako unaoendelea dhidi ya raia wa kigeni wanaoingia hapa nchini kwa shughuli zisizobainika.
Kundi hilo lililojumuisha raia watatu wa Kenya, lilikuwa likisafiri kwa kutumia gari aina ya Toyota Hiace, lenye nambari za usajili KCF 860E, kutoka nchini Uganda hadi mtaa wa Eastleigh Jijini Nairobi, walipokamatwa.
Licha ya juhudi zao za kuwahepa maafisa wa polisi, dereva wa gari hilo baadaye alijisalimisha na kusababisha kutiwa nguvuni kwa washukiwa hao ambao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Tarakwa.
Kikosi cha maafisa wa polisi wa kukabiliana na ugaidi, sasa kimechukua usukani wa kuwahoji washukiwa hao.
Lengo lao ni kubainisha shughuli zao hapa nchini, na kuchunguza uwezekano wa ulanguzi wa binadamu.